Search
Thursday 1 June 2023
  • :
  • :

Marekebisho katika Muungano wa Afrika yatasaidia kuafikia matarajio ya raia, asema Rais Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta amesema kwamba marekebisho ya kitaasisi katika Muungano wa Afrika yatafanikisha weledi wake katika kutimiza mahitaji ya bara hili.

Rais Kenyatta alisema kuwa mchakato wa marekebiksho ya kitaasisi ya Muungano wa Afrika unaendelea kuimarisha uwezo wa mataifa ya Afrika kukabiliana na changamoto na kupanua uchumi kwa ajili kwa manufaa ya wakazi wake.

Rais alisema Kenya vile vile inaunga mkono ushirikishi wa uchumi wa raslimali za bahari katika mfumo mpya wa Muungano wa Afrika.

Kiongozi wa Nchi aliyasema haya katika kikao cha 11 kisicho cha kawaida cha kongamano la Viongozi wa Nchi na Serikali za Muungano wa Afrika katika makao makuu ya Muungano huo jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Lengo kuu la kikako hiki ni mchakato wa marekebisho ya Muungano wa Afrika unaonuia kuifanya taasisi hiyo kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Kenya inaunga mkono mapendekezo ya Baraza Kuu ya kuweka mkakati wa tume yenye wanachama wanane inayohusisha Mwenyekiti, Naibu Mwenyekiti na Makamishna sita,” kasema Rais Kenyatta.

Aidha alisema Kenya inaunga mkono kuanzishwa kwa kiti kisicho cha kugombaniwa cha Mkurugenzi Mkuu ambaye atakuwa na jukumu la ushirikishi wa kazi za wanachama wasio wa kuchaguliwa wa tume ya Muungano wa Afrika.

Kuhusu uchumi endelevu wa raslimali za bahari, Rais alisema ni hatua mwafaka kwani sekta hiyo ina uwezo mkubwa ambao haujazingatiwa kikamilifu katika kuchangia mabadiliko na ukuaji barani Afrika.
Kenya iko katika mstari wa mbele kuhusiana na lengo jipya duniani la kuendeleza uchumi wa raslimali za bahari na inatarajiwa kuandaa kongamano la kwanza kuhusu uchumi huo baadaye mwezi huu.

“Kutokana na haya, kwa mara nyingine natoa mwaliko kwa waheshimiwa viongozi kwenye Kongamano Kuu linalotarajiwa la Uchumi wa Raslimali za Bahari litakalofanyika jijini Nairobi tarehe 26 hadi 28 Mwezi huu, kongamano ambalo litatupa nafasi muhimu kuangazia zaidi maudhui haya muhimu,” kasema Rais.

Rais Kenyatta aidha alishauri Tume ya Muungano wa Afrika kuhakikisha kwamba hata inapoendelea na marekebisho mapya inastahili kujikinga dhidi ya kutekeleza majukumu kwa kurudia rudia ili kuimarisha umoja na weledi kwa mujibu wa taratibu bora.

“Ili kushirikisha kila nchi mwanachana na kanda, tunakubali malengo ya kuheshimu usawa wa jinsia, kugawana mamlaka kwa mzunguko wa kanda, na pia napongeza uongozi wa tume ya Muungano wa Afrika kwa pendekezo la kuwa na asilimia 35 ya vijana katika mchakato wa uchaguzi,” kasema Rais Kenyatta.

Rais alielezea umuhimu wa utekelezaji kamili wa mifumo mipya ili kufanikisha taasisi hiyo barani Afrika ili kutimiza “Afrika tunayoitaka” kama ilivyojikita katika ajenda ya 2063.

Rais Kenyatta alimpongeza mwenzake wa Rwanda, Rais Paul Kagame, ambaye ndiye Mwenyekiti anayeondoka wa Muungano wa Afrika, “kwa msimamo wake na uongozi mwafaka wa mchakato wa marekebisho ya Muungano wa Afrika.”

Vile vile aliipongeza Ethiopia “kwa hatua ya kihistoria ya kisiasa katika kumchagua mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Nchi hiyo, Mheshimiwa Sahle-Work Zewde.”

Akiwa nchini Ethiopia, Rais alijumuika na Waziri Mkuu Abiy Ahmed kwa chakula cha mchana na baadaye akamtembelea Rais Zewde.

Rais Kenyatta alimpongeza Rais Zewde kwa kuchaguliwa kwake na akaahidi kwamba Kenya itaendelea kumuunga mkono.
Huku akimwalika Rais Zewde kuzuru nchini Kenya hivi karibuni, Rais Kenyatta aliahidi kuongoza ujumbe wa kibiashara hadi nchini Ethiopia mwaka ujao kuasisi nafasi za kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa haya mawili.

Kwa upande wake, Rais wa Ethiopia alimpongeza Rais Kenyatta kwa uongozi wake bora katika kanda hii, hasa katika masuala ya kiuchumi, uhusiano wa kijamii, amani na usalama.

Rais Zewde alisema amejifunza mengi kutokana na uhusiano wake wa awali na Rais Kenyatta na akaahidi kufanya kazi hata kwa karibu zaidi na Kiongozi wa Kenya kama ilivyokuwa alipokuwa akihudumu katika Umoja wa Mataifa, jijini Nairobi.

Rais huyo mpya wa Ethiopia aliwasilisha salamu zake kwa Mama wa Taifa Margaret Kenyatta, aliyemtaja kuwa rafiki wake wa karibu na kielelezo kwa viongozi wanawake barani Afrika.

Rais Kenyatta pamoja na Waziri Mkuu Abiy walizungumza kuhusu haja ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Kenya na Ethiopia na kuafikiana kutafuta namna ya kufanya shughuli za pamoja hasa kuanzishwa na kuendeleza maeneo maalumu ya kiuchumi.

Viongozi hao wawili pia walizungumzia amani ya kanda na haja ya kuhakikisha mipaka iko salama kwa biashara.

Rais alimpongeza Waziri Mkuu wa Ethiopia kwa kuwaunga mkono viongozi wanawake kikamilifu kama ilivyojitokeza katika uchaguzi wa hivi majuzi wa Rais wa kwanza wa Ethiopia mwanamke na mabadiliko ya juzi ya Baraza la Mawaziri ambapo wanawake zaidi walipewa nyadhifa za uwaziri.

Waziri Mkuu Abiy alimwambia Rais Kenyatta kwamba Ethiopia imejizatiti kuhakikisha Afrika inakuwa bara lenye umoja na maendeleo. Alisema kwamba chini ya uongozi wake, Ethiopia itasalia kuwa katika nafasi ya mbele kutetea umoja wa Afrika na maendeleo.




Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *