Rais Uhuru Kenyatta leo ameagiza Idara ya Ustawi wa Uvuvi pamoja na Tume ya Ardhi nchini kuchukua hatua za dharura kurudisha ardhi ya maeneo ya kupokelea samaki waliovuliwa ambayo yalinyakuliwa na walaghai.
Rais alisema maeneo yote ya kupokelea samaki baada ya kuvuliwa katika sehemu za pwani, Maziwa Viktoria na Turkana na katika maziwa mengine na mito nchini yapaswa kutwaliwa na kudhibitiwa ifikapo mwezi Machi mwaka ujao.
Wakati huo huo, Rais Kenyatta aliipongeza kampuni moja ya humu nchini iitwayo One Holding Limited kwa kurejesha kwa hiari kwa serikali kituo cha kupokelea samaki waliovuliwa cha Liwatoni na akawahimiza watu wengine ambao walinyakua sehemu kama hizo kuzisalimisha kabla ya serikali kuchukua hatua ya kuzitwaa.
Rais Kenyatta alisema haya alipozindua rasmi Huduma ya Walinzi wa Ukanda wa Pwani huko Liwatoni katika kaunti ya Mombasa ambako pia alitia saini maagizo makuu rasmi ya kuanzisha Shirika la Ustawi wa Uvuvi na Chuo cha Bandari kinachotoa masomo ya masuala ya baharini, akisema taasisi hizo mbili ni muhimu kwa ufufuzi wa matumizi ya raslimali za majini kwa ustawi wa uchumi.
Kabla ya uzinduzi wa kikosi hicho, Rais Kenyatta alishuhudia upakuaji wa tani 150 za samaki wa aina mbali mbali wa thamani ya shilingi milioni 30.
Kwenye hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Naibu wa Rais William Ruto, Rais alisema Huduma ya Kikosi cha Walinzi wa Ukanda wa Pwani, kitashirikiana na vikosi vingine vya ulinzi wa kitaifa, kulinda mipaka ya maeneo ya maji nchini.
“Kwa muda mrefu sasa, tumekuwa na matatizo ya usalama wa baharini ikiwemo shughuli zisizo halali za uvuvi zinazofanywa na wageni kwa kutumia vyombo vya kuvulia samaki kwa wavu chini-chini yaani Kikokoozi, uingizaji bidhaa gushi, uchafuzi wa mazingira ya viumbe hai baharini kwa kuvuja mafuta, utupaji taka zenye sumu na uharibifu wa miamba tumbawe na misitu ya pwani,” kasema Rais.