Search
Thursday 1 June 2023
  • :
  • :

Kenya ni mshirika mkubwa wa Somalia kimaendeleo, asema Waziri Mkuu Khaire

Waziri Mkuu wa Somalia Hassan Ali Khaire ameipongeza Kenya kwa kuwa mshirika nambari moja wa Somalia katika harakati zinazoendelea za kuboresha taifa hilo la Upembe wa Afrika.

Waziri Mkuu Khaire alisema ushirikiano ulioimarika kati ya mataifa haya mawili ni muhimu kwa  ustawi wa kanda ya Afrika Mashariki.

Waziri Mkuu huyo aliyasema haya leo katika Ikulu ya Nairobi alipowasilisha ujumbe wa heri njema na rambi rambi kwa Rais Uhuru Kenyatta kutoka kwa Rais Mohammed Abdullahi Mohamed wa Somalia kufuatia shambulizi la hivi majuzi la kigaidi katika mtaa wa Riverside Drive jijini Nairobi.

Waziri Mkuu Khaire alisema Somalia inatambua wajibu mkubwa unaotekelezwa na Kenya katika kuhakikisha maendeleo na uthabiti wa taifa hilo.

Alimpongeza Rais Kenyatta, akimtaja kuwa shujaa halisi wa katika juhudi za kuiimarisha Somalia.

“Mheshimiwa, wewe ni shujaa wetu katika ujenzi na uimarishaji wa Somalia na tunakuomba uendelee kuongoza juhudi za kuijenga upya yetu,” kasema Waziri Mkuu Khaire.

Waziri Mkuu huyo alimhakikishia Rais Kenyatta kwamba Somalia inaiunga Kenya mkono kwenye vita dhidi ya ugaidi na vurugu zinazosababishwa na itikadi kali.

Alisema shambulizi la kigaidi katika jumba la Dusit D2 limeimarisha zaidi azma ya Mataifa haya mawili katika kukabili ugaidi na vurugu zitokanazo na itikadi kali.

Waziri Mkuu huyo pia aliwapongeza maafisa wa usalama hapa nchini kufuatia hatua yao ya haraka na ya kitaalam ambayo iliokoa maisha ya Wakenya wengi na wageni.

Alisema Somalia imeendelea kuimarika kutoka na usalama na ulinzi unaotekelezwa na kikosi cha AMISON, hii ikiwa ni pamoja na kuandaa Katiba mpya, kupata sarafu mpya sawa na kuboresha taasisi za kiusalama ambazo ni muhimu katika uthabiti wa taifa hilo kiuchumi na kijamii.

Waziri Mkuu Khaire alisema kwa sasa Somalia ni mwenyeji wa zaidi ya Wakenya 50,000 wanaofanya kazi katika sekta mbalimbali za kiuchumi, akiongeza kwamba taifa hilo limeimarisha uwezo wake wa ununuzi na uekezaji kupitia mipango mbalimbali ya maendeleo.

Alisema ukarabati wa Somalia umefanikisha kuanzishwa kwa mipango ya elimu, afya, ustawi wa kijamii na kuipa nchi hiyo nafasi ya kujadili na asasi za kimataifa za kutoa mikopo ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la IMF.




Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *